Jumatano , 15th Feb , 2017

Rapa Nikki Mbishi leo kupitia mtandao wake wa Instgram aliweka ujumbe ukionyesha wimbo wake wa 'I'm sorry JK' kuwa umepigwa marufuku na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), jambo ambalo limeonesha kumgusa mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe.

Ujumbe huo unasomeka kama ifuatavyo

"Baada ya salamu naomba niombe radhi kwa vyombo vyote vya habari kuwa sitoweza kuwapa ushirikiano wowote kuhusu wimbo wangu wa "I'M SORRY JK" uliositishwa na hii ni kwa usalama wao na wangu pia. Napokea simu nyingi sana zikihitaji maelezo juu ya suala hilo ila kiukweli kwa watakaohitaji taarifa kamili wanaweza kufika ofisi za BASATA, naomba nisiwe msemaji tena juu ya jambo hili" aliandika Niki Mbishi 

Kutokana na sakata hilo Zitto Kabwe ameibuka na kuihoji hofu ya serikali kiasi cha kuifungia kazi ya msanii huyo.

"Serikali imepiga marufuku wimbo wa msanii Nikki Mbishi. Wallah nilidhani ni utani kumbe kweli, serikali hii inachoogopa ni nini? Dah kua uyaone" aliandika Zitto Kabwe kupitia mtandao wake wa Twitter. 

Mbali na hilo rapa Nikki Mbishi ameendelea kuwaomba watu wasiendelee kusambaza wimbo huo na kama wao watafanya hivyo basi yeye hatahusika katika suala hilo 

"Kwa yeyote atakayeendelea kuusambaza au kuucheza popote pale mimi sitahusika naye maana 'technology' iko huru popote duniani na siwezi kuzuia watu wasiupate kwa kuwa ushasambaa, hivyo chukua tahadhari ili usijikute mikononi mwa sheria, naomba msubiri ujio wangu mpya wa singeli na aina nyingine za muziki kama naija, mchiriku" alisisitiza Nikki Mbishi