Yaliyomkuta Harmonize ndiyo yamemkuta na Ibraah Tz

Ijumaa , 16th Oct , 2020

Mara kadhaa msanii na CEO wa lebo ya Konde Gang, Harmonize amekuwa akipata usumbufu wa kutolewa na kurudishwa kwa video za nyimbo zake kwenye mtandao wa YouTube baada ya kupandisha video hizo kwenye mtandao huo.

Msanii Ibraah Tz upande wa kulia na kushoto ni Harmonize

Sasa tatizo hilo limemtokea pia msanii wake Ibraah Tz ambaye akaunti yake YouTube haipatikani na imefungiwa kwa sasa kwenye mtandao huo.

Ukiingia kwenye 'profile' ya Instagram anayotumia msanii huyo ameweka 'link' ya video ya wimbo wake wa nitachelewa ila ukibonyeza link hiyo kuna maneno ya kiingereza yanayomaanisha kuwa "Video hii haipatikani tena kwa sababu akaunti ya YouTube inayohusishwa na video hii imesimamishwa".

Maneno hayo yanadhihirisha kuna tatizo kwenye akaunti yake hadi kufungiwa na mtandao wa YouTube, mara nyingi tatizo hilo husababishwa na ukiukaji wa miongozo ya jumuiya au masharti kama kuchapisha video zisizo na maadili, chuki, unyanyasaji au kesi za haki miliki.

Tayari msanii Harmonize ameshakutana na tatizo la kufutiwa video za nyimbo zake kama uno, bedroom na album yake ya Afro East kisha kurudishwa baadaye.