"Wanakuonea wivu hadi ukisemwa vibaya" - Nanauka

Alhamisi , 7th Jan , 2021

Mhamasishaji Joel Nanauka amefunguka kuhusu suala la wivu ambalo linawatesa watu wengi kwa kusema, wivu ni hisia inayompata mtu pale anapoona mwingine anapata au kufanikiwa kisha yeye kuumia na kuchukia, pia wapo wenye wivu wa kimya kimya na wanaosema.

Mhamasishaji Joel Nanauka

Aidha Joel Nanauka amefika mbali zaidi kwa kutaja sababu nne za watu kuoneana wivu ambapo ni 

Kustahili

Sababu ya kwanza watu huona kwamba yule aliyepata hastahili, wapo ambao wameshajihesabia kuwa wao ndiyo wanatakiwa kupata kitu fulani au kila kitu halafu wewe hustahili sasa hali hiyo hupelekea kumjengea wivu na chuki dhidi yako.

Kufanya kitu ambacho wao wamefeli 

Sababu ya pili ya watu kuona wivu ni kufanya kitu ambacho wao wamefeli na anapomuona mtu mwingine anafanikiwa kwenye hiko kitu ambacho yeye umekishindwa basi anaona kama anahukumiwa kimya kimya anaanza kukuonea wivu.

Kufanikiwa kwa ulichotamani kukifanya

Kuna watu wanakuonea wivu  kwa sababu hawajawahi kukifanya hiko kitu ila kinachotokea wewe unapokifanya yeye kinamuumiza na kutamani kama angekuwa yeye kwenye hiyo nafasi hivyo inamuumiza na kumletea majuto ndani yake. 

Tamaa ya kuwa juu siku zote 

Kuna watu ambao inawauma sana mtu mwingine akisifiwa inawezekana hata hicho kitu yeye hana uwezo nacho kabisa yote ni kwa sababu hutaka yeye ndio kuwa juu, sasa shauku hiyo humfanya mtu aone wivu kwa mwingine maana wapo watakuonea wivu hata ukisemwa kwa mambo mabaya yeye anachukia tu.