Jumatano , 12th Apr , 2017

Msanii wa Injili nchini Upendo Nkone amekiri kuwa ni kweli alikuwa anatumia mkorogoro (anajichubua ngozi) lakini hivi sasa ameacha kufanya hivyo baada ya mashabiki wake kumjia juu na kutaka aachane na mambo hayo ya kujichubua.

Upendo Nkone - Msanii wa Injili

Upendo Nkone amesema hayo kupitia kipindi cha Kikaangoni kinachofanyika kupitia ukurasa wa facebook wa EATV kila siku ya Jumatano kuanzia saa nane mchana mpaka saa kumi jioni.

Akitaja sababu kuu tatu za kuacha kutumia mkorogo, Upendo amesema sababu ya kwanza ni kwamba aligundua kujichubua ni kumkosoa Mungu aliyemuumba, ya pili ni kwamba aligundua kuwa mkorogo ulikuwa unaathiri ngozi yake na sababu ya tatu ni mashabiki zake kuwa hawapendi kumuona akiwa anatumia mkorogo.

"Kwa sasa nimeacha kujichubua kabisa, ni kweli nilikuwa najichubua lakini mashabiki wangu walikuwa hawapendi, walikuwa wakinipigia simu na kunikataza huku wakisema niachane na tabia hiyo na mimi nikaamua kuacha" amesema Upendo Nkone 

Upendo anasema sababu kubwa iliyompelekea yeye kujichubua ni kutaka kuondoa michirizi ambayo ilikuwa ikimtoka mwilini hivyo kuna mtu alimshauri kuwa akitumia dawa fulani ingetoka na kweli baada ya kuanza kutumia michirizi hiyo ilianza kutoka lakini na rangi yake ilianza kubadilika na kuanza kuwa mweupe, kitu ambacho kilifanya mashabiki wake kuanza kumkataza na kutopendezwa na rangi yake hiyo. 

Upendo Nkone akiwa Kikaangoni

Mume wa Chibalonza

Katika hatua nyingine, moja kati ya mashabiki waliouliza maswali walitaka kujua kama ni kweli ameolewa na mume wa aliyekuwa mume wa mwanamuzi wa Injili marehemu Angela Chibalonza ambapo amakanusha huku akifafanua kuwa mwanaume huyo amewahi kumpelekea maombi ya kumuoa, lakini bahati mbaya huyu mume aliyenaye kwa sasa akawa amemuwahi.

Kuolewa tena

Waliotaka kujua ni kwanini aliolewa tena, amesema aliamua kuolewa tena kwa ajili ya kusaka heshima na imani kwa watu, maana kwa huduma anayoifanya anaamini watu wasingeweza kumuamini kama kweli anakaa bila mwanaume

"Niliamua kuolewa kwa sababu niliona kwa huduma yangu nahitaji mtu, maisha ya ujane watu wanakuwa hawaniamini, hata nikimaliza kuimba watu wanajiuliza hivi huyu kweli hana mtu, halafu kuolewa ni heshima, mume ni kivuli, mume ni baraka kutoka kwa Mungu, sasa hivi naitwa Mama Mchungaji"

Akitaja wasanii watatu wa injili anaowakubali, amesema anawakubali zaidi Bahati Bukuku, Christina Shusho pamoja na Rose Mhando huku akiweka wazi kuwa hana mpango wa kufanya kolabo na Rose Mhando, wala hajafikiria kitu kama hicho.

Kuna waliotaka kusikia maoni yake kuhusu Mchungaji Josephati Gwajima ambapo amewajibu kuwa hawezi kusema chochote kwa kuwa mchungaji huyo ni mtumishi wa Mungu na ana imani yake, kwahiyo anajijua yeye na Mungu wake.

Msikilize hapa katika sehemu ya kipindi cha Kikaangoni