Jumanne , 25th Jul , 2017

Mwanamuziki anayefanya vizuri na ngoma yake ya 'Libebe', Beka Flavour amefunguka na kusema Aslay siyo msanii mkubwa wa kumuangalia wakati anafanya kazi zake na badala yake Alikiba ndiye kioo chake kwa Tanzania.

Msanii Beka Flavour

Beka amelazimika kusema hayo baada ya kuwepo minong'ono kuwa huenda anamuogopa msanii huyo ambaye zamani walikuwa wakifanya kazi pamoja kama kundi la 'Yamoto Band' kabla ya kila msanii kuanza kusimama mwenyewe.

"Mimi natoa nyimbo zangu kulingana na jinsi ambavyo nimepanga ratiba yangu na uongozi wangu. Sijashindwa kuachia wimbo eti kwa sababu Aslay katoa ngoma mpya ila matatizo niliyopata ya kupelekwa polisi ndiyo yaliyonifanya nisogeze vitu mbele," Beka alifunguka mbele ya kamera za eNewz

Beka aliongeza kuwa "Aslay siyo msanii mkubwa kusema kwamba mimi nimuogope au nimfikirie. Hapa nchini msanii mkubwa ni Alikiba na ndo kama kioo najitazama lakini siyo Aslay. Mimi natazama wasanii wakubwa nje ya nchi lakini siyo ndugu yangu".

Pamoja na hayo Beka amedai hataweza kumvumilia tena msanii huyo ambaye amefululiza kutoa nyimbo nyingi hivi karibuni endapo ataachia tena kazi mpya.

"Nimepanga kuachia wimbo mpya wiki mbili zijazo lakini kama Aslay akiachia tena kazi mpya sitaweza kumvumilia na mimi nitaachia mashine ili zipambane mbele kwa mbele maana mimi nimeshapanga ratiba zangu na siwezi kuzivunja," aliongeza.