Jumamosi , 23rd Sep , 2017

Baadhi ya wasanii nchini Kenya wanaendesha kampeni ya kuchangia matibabu ya muigizaji wa filamu nchini humo Luwi Cappelo, ambaye alipata ajali ya gari na kulazwa hospitali.

Luwwi Cappelo

Wasanii hao akiwemo Nyota Ndogo wanatarajia kufanya tamasha ambalo pesa ambazo zitapatikana, ziweze kugharamia matibabu ya Luwi Cappelo ambaye bado yupo hospitali mjini Mombasa nchini Kenya.

"Mungu amemsaidia ameamka anaendelea vizuri na kwakweli amepewa ruhusa ya kwenda nyumbani ila hawezi kuondoka kabla hajalipa bili ya hospitali, yani kachoka na hospitali, wapenzi wangu mashabiki wangu popote mulipo chochote ulichonacho tafadhali msaidieni huyu kaka kwenye hiyo namba, tuma chochote yani, anae omba hatoi masharti, chochote wapenzi atoke hospitali, hii juma mosi tutakua tunajitokeza pale coast car park kwa ajili ya Luwi, ukipata muda tafadhali njoo na chochote", ameandika Nyota Ndogo kwenye ukurasa wa instagram.

Luwi Cappelo ambaye pia ameshawahi kuigiza kwenye mchezo wa 'Siri za Familia' wa hapa nyumbani unaorushwa na East Africa Television, alipata ajali mbaya ya gari iliyopelekea kupoteza fahamu, akiwa anatoka Mombasa kurejea jijini Nairobi nchini Kenya.