Alhamisi , 20th Apr , 2017

Msanii wa filamu nchini, Jacob Steven maarufu kama JB amefunguka ya moyoni na kusema kwamba ni kweli sinema zao zina mapungufu mengi lakini isiwe sababu ya wao kuacha kudai haki zao wanazoamini kuwa wananyonywa katika pato la mauzo.

Msanii wa filamu nchini Jacob Stephen

Hayo yameibuka baada ya kelele nyingi katika mitandao ya kijamii ikiwasema waigizaji pamoja na watayarishaji wa filamu nchini kukosa ubunifu wa kutosha na sasa kushinikiza serikali izuie kuingiza filamu zinazotoka nje ya nchi.

“Kwenye shida mimi sitajali nani ananisaidia ili mradi anagusa maslahi yangu, ugali wangu. Nakiri sinema zetu zina mapungufu mengi lakini hilo siyo sababu za kuacha kudai haki zetu, ni kama mgonjwa akiumwa leo anapelekwa kwa mganga kesho anapelekwa kuombewa, anatetea roho yake”. Ameandika Jb kupitia mtandao wake wa kijamii instagram

Vilevile JB, amesema hakuna aliyesema filamu za nje zifungiwe ila wanachotaka ni zifuate utaratibu kama wanavyofuata wao wenyewe.

“Ngoja tumalize hili tusichanganye na pia hakuna aliyesema zifungiwe hapana zifuate utaratibu kama sisi tunavyofuata hizo hizo ‘movie’ zetu mbovu ndiyo zinatuwezesha kuishi lakini pia lazima mfahamu biashara hii ni kubwa kuliko mnavyodhania, muvi mbili zinanitosha kuishi kwa mwaka mzima, ushawaza ni kiasi gani ?”. Alisisitizia JB

Kwa upande mwingine amewashukuru wananchi kwa kumpa ushirikiano katika kazi zake zaidi ya 50 kwa miaka 20 tangu anze fani hiyo.