Jumanne , 21st Mar , 2017

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeahirisha kesi ya dawa za kulevya inayomkabili msanii Agnes Gerald Waya maarufu kama Masogange baada ya kutohudhuria kesi hiyo mahakamani.

Agnes Gerald

Kesi hiyo ambayo imetajwa kwa mara ya kwanza mbele ya hakimu mkazi wa Kisutu Wilbard Mashauri wakili wa serikali Adolf Mkini amesema kuwa mshtakiwa anakabiliwa na mashtaka mawili ya kutumia dawa za kulevya aina ya Heroin na Oxazepham.

Ameeleza kuwa mshitakiwa anadaiwa kuwa kati ya Februari 7 na 14, 2017 katika maeneo yasiyojulikana ndani ya jiji la Dar es Salaam  alitumia dawa za kulevya aina ya Heroin (Diacety Imophine) na kuwa kati ya Februari 7 na 14, 2017  alitumia dawa za kulevya aina ya Oxazepam.

Mshitakiwa anadaiwa kufanya makosa hayo chini ya kifungu cha 18 (a) cha sheria ya kupambana na dawa za kulevya namba 5 ya mwaka 2015 na kuwa uopelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika licha ya mshtakiwa kutokuwepo mahakamani hapo.

Hata hivyo  wakili wa Masogange, Nictogen Itege aliwasilisha udhuru mahakamani hapo juu ya mteja wake kutokuwepo.

Licha ya maelezo hayo Hakimu Mashauri alimtaka mshtakiwa kuheshimu masharti ya mahakama na kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 20, mwaka huu mshitakiwa yupo nje kwa dhamana.