Jumatatu , 23rd Nov , 2020

Msanii Kala Jeremih amefunguka kusema wamenusurika kupata ajali na Sholo Mwamba wakiwa safarini kurejea Dar Es Salaam wakitokea Jijini Dodoma.

Kushoto ni Kala Jeremiah, kulia ni Sholo Mwamba

Akizungumiza kuhusu tukio hilo kwenye kipindi cha Planet Bongo ya East Africa Radio Kala Jeremiah amesema kuwa 

"Tumenusurika ajali tulikuwa kwenye speed tukasikia kishindo nikajua tairi limebast kumbe ni diff imekula bearing ambayo ikakata mawasiliano ya tairi, tunashukuru Mungu dereva akai-control gari vizuri tukajikuta tunaning'inia kwenye ukingo wa barabara" amesema Kala Jeremiah 

Aidha ameongeza kusema "Nilikuwa mimi Sholo Mwamba, meneja wake, Dj Tittoh na dereva wetu ambaye tunajiuliza tumpe zawadi gani kama kamati, kwa jinsi watu waliyoona walisema sio dereva wa nchi hii, kilichotokea pale kuokoka ilikuwa kama ni mkono wa Mungu tu"

Ikumbukwe mwezi Septemba mwaka huu wasanii wengine ambao ni Belle 9, Lulu Diva na Bonge la Nyau walipata ajali ya gari maeneo ya Chalinze wakati wanarejea Dar Es Salaam wakitokea Iringa kwenye kampeni za Chama Cha Mapinduzi.