Faiza Ally amtuliza Sugu baada ya kukosa Ubunge

Alhamisi , 29th Oct , 2020

Mfanyabiashara Faiza Ally amempa moyo na kumuunga mkono aliyekuwa mpenzi wake wa zamani na baba mtoto wake Joseph Mbilinyi 'Mr II Sugu' baada ya kushindwa nafasi ya Ubunge kwenye Jimbo la Mbeya Mjini ambapo limekwenda kwa Dkt Tulia Ackson wa Chama Cha Mapinduzi.

Picha ya mfanyabiashara Faiza Ally na Joseph Mbilinyi 'Mr II Sugu'

Kupitia ukurasa wake wa Instagram Faiza Ally ameandika maneno ya kumtia nguvu mzazi mwenzake huyo kufuatia kushindwa kutetea nafasia yake ya Ubunge wa Jimbo hilo kwa kura 37,561 dhidi ya kura 75,225 ambazo amezipata Dkt Tulia Ackson.

"Tulikupendaga, tuliendelea kukupenda, tunakupenda zaidi na tutakupenda kila siku , machoni mwetu na kwenye mioyo yetu wewe ni mshindi toka mtoto mpaka utazeeka na mpaka siku ya mwisho itakua hivyo hakuna kitakacho badilika, mimi na familia tunakutumia salamu za upendo tunatamani kuwepo ulipo tusheherekee maisha pamoja  kwa sababu wewe ni mshindi kwetu, najivunia wewe baba Sasha" ameandika Faiza Ally 

Joseph Mbilinyi anawakilisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) aliongoza Jimbo la Mbeya Mjini kuanzia mwaka 2010 hadi 2020, ambapo kuanzia sasa litaongozwa na Dkt Tulia Ackson kama ambavyo Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Mbeya Mjini alivyomtangaza kushinda nafasi ya Ubunge wa Jimbo hilo.