Jumamosi , 21st Oct , 2017

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, amewataka viongozi wa Shirika Hodhi la Rasilimali za Reli (RAHCO), kuwa katika eneo la mradi wa ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR) muda wote.

Waziri amesema hiyo itasaidia kuhakikisha mkandarasi anapata ushirikiano wa kutosha na hivyo kuwezesha mradi kukamilika kama ilivyopangwa ambapo takribani shilingi trilioni 2.8 zinatarajiwa kutumika.

Profesa Mbarawa amesema hayo alipokagua ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), inayojengwa usiku na mchana kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro  yenye urefu wa KM 205 na kuzungumzia kuridhishwa na kasi ya ujenzi huo.

Pia Mh. Waziri  amemuagiza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa RAHCO Mhandisi Edward Malima, kuhakikisha wanafunzi wa uhandisi wanapata nafasi ya kutosha ya kushiriki kwa vitendo katika ujenzi huo ili kuiwezesha nchi kuwa na wataalamu wa kutosha wenye uzoefu kwenye ujenzi na usimamizi wa miradi ya reli.

Naye  Mhandisi Edward Malima, amempongeza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa kufanya ziara ya kustukiza usiku ambayo imechochea hamasa kwa wafanyakazi na mkandarasi na kuahidi  kumsimamia mkandarasi kikamilifu ili mradi huo ukamilike kwa wakati na uwiane na thamani ya fedha.