Jumapili , 22nd Nov , 2020

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Aboubakar Kunenge, amewaelekeza baadhi ya wakazi wa eneo la Kunduchi Mtongani ambao nyumba zao zimepitiwa na ujiuji wa volcano ya tope linalofuka kutoka ardhini kuhama Mara moja ili kujikinga huku Serikali inaendelea kufanya utafiti juu ya athari iliyotokea.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Aboubakar Kunenge

RC Kunenge akiongozana na wajumbe wa kamati ya usalama ya Mkoa, leo, wamefika Katika eneo hilo na kushuhudia uwepo tope linalotoka ardhini na kupanda Katika uso wa ardhi jambo lililosababisha baadhi ya nyumba kutitia, kupasuka nyufa na mifugo kutitia hivyo kuzua taharuki kwa wakazi wa eneo hilo.

             RC Kunenge wa tatu kushoto akiwa katika mmoja ya nyumba iliyopata athari ya 'volcano ya tope'

Kutokana na hali hiyo RC Kunenge amemuelekeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, kuweka alama za hatari Katika eneo hilo wakati Serikali chini ya Taasisi ya Geologia na utafiti wa Madini Tanzania ukiendelea kupitia ukubwa wa eneo lililoathirika.

Pamoja na hayo RC Kunenge amesema Serikali inaangalia utaratibu wa kuwapatia wananchi wa eneo hilo viwanja vingine ili waweze kuendelea na maisha kama awali.

Kwa upande wake Mtafiti kutoka Taasisi ya Geologia na utafiti wa Madini Gabriel Mbogoni amesema matokeo ya awali wamebaini chanzo cha tope hilo ni mgandamizo uliosababishwa na uwiano wa maji na chembechembe za udongo kuharibika na kusababisha tope ambalo linasukumwa kutoka chini kwenda kwenye uso wa ardhi.

Aidha Bwana Mbogoni amesisitiza kuwa tope hilo wamelipima na kukuta likiwa na joto la kawaida hivyo halina uhusiano wowote na ile volcano inayorusha majivu na Moto utokanao na miamba iliyoiva hivyo eneo hilo kwa Sasa ni tete na halifai kwa shughuli za Ujenzi Wala makazi.