Jumapili , 7th Feb , 2021

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani ametaka Meneja wa Kituo cha Kupoza na Kusambaza umeme cha Kinyerezi I, Ubungo I pamoja na Mhandisi Mkuu wa Kinyerezi II, Kinyerezi I, na Ubungo I, wasimamishwe kazi na wachunguzwe kwa uzembe.

Kulia ni Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani akizungumza na baadhi ya wahandisi wanaoendesha Kituo cha Umeme cha Ubungo, wakati wa ziara ya kukagua kituo cha umeme cha Kinyerezi I, Kinyerezi II na Ubungo.

Dkt.Kalemani ametoa maagizo hayo baada ya kubaini uzembe uliofanyika katika vituo hivyo wakati wa ziara yake Jijini Dar es Salaam, ya kukagua vituo hivyo na  kuzungumza na Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) 

“Haiwezekani Meneja na Mhandisi Mkuu wote wasiwepo katika vituo vyenu vya kazi bila sababu za msingi, mitambo yote inafanyiwa ukarabati kwa wakati mmoja Hapana, hii haiwezekani ni uzembe wa hali ya juu lazima wachunguze na waondolewe katika nafasi zao za kazi", alisema Dkt. Kalemani.

Aidha Waziri Kalemani alitoa siku kumi na nne (14) kwa Bodi hiyo kuwafanyia uchunguzi mameneja na wahandisi wakuu hao na kumpatia majibu stahiki pamoja na kuiigazi Bodi ya TANESCO kuhakikisha kuwa mtaalamu wa kuunga kifaa cha kuongeza umeme(Buster) kilichopata hitilafu katika Kituo cha Kupoza umeme cha Kinyerenzi I, anapatikana na kufunga kifaa hicho ndani ya siku tatu (3) na kituo hicho kizalishe umeme kama ilivyokuwa hapo awali.

Sambamba na hilo, aliwataka wataalamu wanaofanya ukarabati katika vituo hivyo kufanya kazi hiyo usiku na mchana ili kukamilisha matengenezo hayo haraka, na vituo hivyo kuzalisha megawati zote za umeme unaotakiwa katika vituo husika.