Ijumaa , 20th Nov , 2020

Mahakama ya Uhujumu Uchumi, imemuhukumu kwenda jela kutumikia kifungo cha miaka 30 mfanyabiashara Yanga Omari, maarufu kama rais wa Tanga,baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kusafirisha na kuuza madawa ya kulevya aina ya Heroin kiasi cha gramu 1052.63.

Mahakama Kuu Kanda ya Tanga

Akitoa hukumu hiyo Jaji Imaculata Banzi wa Mahakama hiyo, amesema ameridhika na ushahidi uliotolewa, ambapo upande wa mshtakiwa uliowakilishwa na Mohamed Kajenge uliiomba mahakama impunguzie adhabu  kwa sababu ni kosa lake la kwanza na  ana umri mkubwa zaidi ya miaka 60 na anategemewa na familia yake huku pia akidaiwa kuwa na shinikizo la damu.

Hata hivyo, Jaji Banzi amesema gari aina ya Land-Cruser V8 na silaha yake vilivyokuwa vikishikiliwa na serikali virejeshwe kwa familia yake ikiwemo madawa aliyokamatwa nayo yateketezwe mara moja.
Yanga anadaiwa kwamba mnamo Agosti, 2018 na wenzake  wawili walikamatwa mtaa wa Bombo jijini Tanga, wakitaka kusafirisha dawa hizo za kulevya.

Faraja Nchimbi ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi  kutoka, ofisi ya Taifa ya mashtaka ambaye pia anasimamia mashauri mbalimbali na masuala yanayohusiana na dawa za kulevya, ugaidi pamoja na masula ya makosa ya baharini, amesema kuwa uamuzi huo ni sehemu ya jitihada ya serikali katika kuhakikisha vita dhidi ya dawa za kulevya inapiganiwa vilivyo kwa kuzingatia sheria kali zilizopo.