Alhamisi , 8th Apr , 2021

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere ameisoma ripoti yake ya mwaka wa fedha 2020/21 mbele ya waandishi wa habari leo Aprili 8, 2021 jijini Dodoma na kubainisha baadhi ya taasisi zikiwemo wizara zilizofanya manunuzi nje ya utaratibu.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere (kushoto)

CAG Kichere amezitaja baadhi ya wizara hizo ambazo zimefanya manunuzi ya bidhaa na huduma nje ya mpango wa manunuzi wa mwaka kuwa ni Wizara ya Afya, Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Utalii, Mifugo na Uvuvi pamoja na taasisi nyingine kama Tume ya taifa ya Uchaguzi (NEC).

''Ununuzi uliofanyika nje ya mpango wa mwaka wa manunuzi, jumla ya taasisi 7 ambazo ni TRA, Wizara ya Afya, Zimamoto, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Manispaa ya Morogoro, Wizara ya mambo ya Nje, Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilifanya ununuzi wa vifaa na huduma wa zaidi ya shilingi Bil 15.129,'' ameeleza CAG Charles Kichere.

Mbali na ripoti katika eneo hilo la manunuzi, CAG pia amezitaja Halmashauri, Manispaa pamoja na Taasisi ambazo zimepewa hati mbaya.

''Mwaka huu nimetoa hati mbaya kwa Halmashauri za Wilaya Shinyanga, Singida, Itigi na Igunga, Wilaya ya Sikonge, Urambo, Momba, Manispaa ya Tabora, Hospitali ya Rufaa Morogoro, Tume ya UNESCO,” amesema CAG Charles Kichere.

Ikumbukwe kuwa Machi 28, 2021 CAG Charles Kichere aliisoma ripoti hiyo na kuiwasilisha kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.