Waumini waangukiwa na kanisa, polisi yataja chanzo

Ijumaa , 20th Nov , 2020

Waumini 18 wa Kanisa la Free Pentekoste, lililopo Kijiji cha Kamsisi Kata ya Kamsisi wilaya ya Mlele mkoani Katavi, wakiwamo watoto na watu wazima wamejeruhiwa baada ya kuangukiwa na ukuta wa kanisa hilo wakati ibada ikiendelea, kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha mkoani humo.

Kanisa lililoanguka mkoani Katavi

Taarifa hiyo imetolewa leo Novemba 20, 2020, na Kamanda wa polisi mkoani humo, Benjamini Kuzaga, ambapo amesema kuwa  chanzo cha maafa hayo ni mvua kubwa iliyonyesha ikiwa imeambatana na upepo mkali, hali iliyopelekea kulowa kwa kuta za kanisa hilo na kisha kuanguka.

Akiendelea kutolea ufafanuzi wa maafa hayo Kamanda Kuzaga amesema kuwa kati ya watu 18 waliojeruhiwa 7 ni watoto na 11 ni watu wazima.

Jeshi la Polisi mkoa wa Katavi, limewaasa wananchi kuwa makini katika kipindi hiki cha msimu wa mvua kwa kuchukua tahadhari katika makazi wanayoishi.