Ijumaa , 4th Dec , 2015

Maofisa nane wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), akiwemo Kamishna wa Forodha wa mamlaka hiyo Tiagi Masamaki (56) wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kutoa makontena 329 bandarini.

Mshitakiwa namba moja katika kesi ya kuhujumu uchumi, Tiagi Masamaki (katikati) na washitakiwa wenzake wakitoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam

MAOFISA wanane wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), akiwemo Kamishna wa Forodha wa mamlaka hiyo Tiagi Masamaki (56) wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kutoa makontena 349 bandarini bila ya kulipiwa kodi na kuisababishia serikali hasara ya sh. bilioni 12.7 za kitanzania.

Ukimuondoa Masamaki maofisa wengine waliopandishwa kortini ni Habibu Mponezya (45) Meneja wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja,Bulton Mponezya (51).

Wakili wa Serikali Mwandamizi Christopher Msigwa akisaidiana na Peter Vitalis ameeleza mbele ya Hakimu Mkazi Huruma Shahidi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwa watuhumiwa hao wanatuhumiwa kwa makosa mawili.

Alidai makosa mawili ya uhujumu uchumi ni kula njama ya kuidanganya serikali na kuisababishia serikali hasara. Kesi hiyo ni namba 35/2015 ya uhujumu uchumi.

Ilidaiwa katika shitaka la kwanza katika tarehe tofauti kati ya Juni 1 na Novemba 17 mwaka huu, sehemu isiyojulikana ndani ya Jiji la Dar es Salaam kwa pamoja walikula njama ya kuidanganya serikali kuwa sh. bilioni 12.7 zimetolewa kwa kutoa makontena 349 katika Bandari Kavu ya Azam, baada ya kodi zote kutolewa.

Katika shitaka la pili, washitakiwa wanatuhumiwa katika ya Juni Mosi na Novemba 17 mwaka huu ndani ya Jiji la Dar es Salaam walishindwa kutimiza majukumu yao kwa namna inavyotakiwa na kusababisha Serikali kupata hasara ya sh. bilioni 12.7.

Baada ya washtakiwa hao kusomewa makosa yao, Hakimu Shahidi aliwaeleza kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, kwa hiyo hawatakiwi kujibu chochote kama kweli au si kweli.

Aliongeza kuwa Mahakama Kuu ndiyo ina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, kwa hiyo kama wanataka dhamana wapeleke maombi ya dhamana katika mahakama hiyo.