Alhamisi , 11th Feb , 2016

Mamlaka ya Mapato nchini Tanzania(TRA), imeikabidhi Kampuni ya Udalali ya Yono iwafilisi wateja 24 wanaodaiwa kodi ya shilingi Bilioni 18.95 baada ya kutorosha makontena ya mizigo kwenye bandari kavu (ICD) ya Azam.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya YONO, Bw, Stanley Yono Kevela

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo Yono Kevela amesema hayo jana na kuongeza kuwa wamepewa amri na TRA, ya kisheria ya kukamata mali za wadaiwa na kuwafilisi ili kulipa kodi wanazodaiwa.

Bw. Kevela amesema baada ya kupata kazi hiyo wameona ni busara kutangaza na kuwapa siku 14 kulipa kodi wanazodaiwa na kwamba baada ya muda huo kumalizika hatua za kukamata mali za wadaiwa zitaanza.

Majina ya wadaiwa hao yametolewa jana kwa vyombo mbalimbali vya habari na kampuni hiyo ya udalali baada ya TRA, kuwakabidhi kazi ya kuwafilisi kutokana na kushindwa kutekeleza wajibu wao baada ya kupewa muda wa kufanya hivyo.

Kevela amesema ili kurahisisha kazi Kampuni ya Said Salim Bakharesa(SSB), ambayo ndiyo mmiliki wa bandari kavu pamoja na kampuni ya Regional Cargo Service wanapaswa kutoa ushirikiano kuhakikisha wadaiwa hao wanalipa kodi walizokwepa.