Jumatano , 22nd Oct , 2014

Watu watatu wamekufa na wengine hawajulikani walipo baada ya kuzuka mapigano ya kugombea ardhi kati ya Wafugaji na Wakulima katika kijiji cha Kinyinya kata ya Nyamtukuza wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma.

Mapigano hayo yametokea jana Jumatatu (Oktoba 20) katika eneo la mashambani katika kijiji hicho, baada ya mfugaji mmoja kuuawa na mifugo yake kukatwakatwa Jumatano iliyopita, tukio lililosababisha mapigano mengine yaliyopelekea vifo vya watu wawili ambao waliuawa na kuchomwa moto huku wananchi wengine ambao wanaendesha shughuli katika eneo hilo wakikimbia kusikojulikana.

Wakizungumzia tukio hilo wananchi wamesema chanzo cha ugomvi huo ni ardhi ambapo wafugaji kutoka mikoa ya Geita na Shinyanga wanadaiwa kupewa ardhi kinyume cha utaratibu katika kijiji hicho na uongozi wa kijiji ambao hata hivyo umekanusha kutoa ardhi hiyo.

Akizungumza na wananchi baada ya kufika katika kijiji hicho, kaimu mkuu wa wilaya ya kakonko Venance Mwamoto, ambaye ni mkuu wa wilaya ya Kibondo amesema serikali itawatafuta watu wote waliohusika na mauaji hayo na kuwachukulia hatua, ambapo amesisistiza wakulima na wafugaji kuishi kwa upendo na kutolifanya tukio hilo kuwa la kisiasa katika kipindi hiki ambacho serikali inalishughulikia.