Ijumaa , 26th Dec , 2014

Wananchi wa kijiji cha Sokon Two Wilayani Arumeru mkoani Arusha wamelazimika kuandamana hadi kwenye ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha kupinga hatua ya utolewaji wa vibali vya ukataji miti katika eneo la chanzo cha maji.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Bw. Juma R. Iddi, akitoa maelezo mafupi kwa Katibu Mkuu Kiongozi (hayupo pichani).

Wakiwa na jazba wananchi hao wakiongozwa na Mwenyekiti wao wa kijiji huku baadhi yao wakiwa na fimbo wakidai kutaka kuchukua hatua za kumchomea nyumba na kumchapa viboko sabini aliyekata miti hiyo, wamesema uharibifu huo wa vyanzo vya maji umesababisha kupungua kwa kiasi kikubwa huduma hiyo muhimu.

Hata hivyo baada ya malumbano yaliyochukua takribani saa mbili Mwenyekiti wa kijiji akawashauri wananchi hao kutokuchukua sheria mkononi na badala yake wakalazimika kuandamana kuelekea kwenye ofisi ya halmashauri ambapo walikutana na mwanasheria wa halmashauri hiyo ya Arusha ambaye anawaahidi kuchukua hatua za haraka kuwawajibisha wote waliohusika.

wanaharakati wa mazingira wanalielezea tukio hilo kuwa ni hatua muhimu kwa wananchi kusimamia kikamilifu rasilimali zinazowazunguka bila kuiachia serikali peke yake.