Ijumaa , 27th Nov , 2020

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu watu tisa kulipa faini ya Shilingi elfu hamsini (50,000), kila mmoja au kutumikia kifungo kwa miezi mitatu baada ya kukutwa na hatia ya kuondoka nchini kinyume cha sheria ya uhamiaji.

Pichani: Mfano wa pingu

Waliohukumiwa ni Shabani Saidi, Masoud Simba, Ramadhani Khamisi, Yassin Mbonde, Kioma Samuel, Chris Mrope, Michael Sempindu, Yusuf Kecha na Yasin Hamis.

Hukumu hiyo imetolewa hii leo na Hakimu Mkazi Mkuu Janeth Mtega baada ya washtakiwa hao kukiri kutenda kosa hilo.

Awali, Wakili wa Serikali Shija Sitta, aliwasomea mashtaka yanayowakabili kuwa Novemba 11, mwaka huu washtakiwa walikamatwa katika uwanja wa taifa wa Mwalimu Julius Nyerere baada ya kurudishwa kutoka nchini Afrika Kusini   na ndipo walipopelekwa katika ofisi za uhamiaji Jijini Dar es salaam kwa ajili ya mahojiano.

"Kwa kosa walilolitenda washtakiwa la kuondoka nchini bila kufuata kanuni na taratibu maalumu, naiomba Mahakama yako tukufu iwape adhabu kali ili iwe funzo kwa wengine" amesema Wakili Sitta.

Hata hivyo, kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, washtakiwa walijitetea mbele ya Mahakama kuwa wanaomba wapunguziwe adhabu kwa sababu wamekiri kosa lao na kutorudia Tena kutenda kosa, baada ya kupewa nafasi na hakimu Mtega  ya kusema chochote.