Alhamisi , 2nd Jun , 2016

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli amesema kwamba baadhi ya wanafunzi waliofukuzwa Chuo Kikuu Dodoma UDOM kati ya wale 7,802 walistahili kwa kuwa wengi walikuwa na Divion 3 na 4 na hawakuwa na vigezo vyakusoma Stashahada.

Rais Magufuli ameyasema hayo wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa maktaba ya kisasa chuo kikuu cha Dar es salaam ambayo itajengwa kwa mkopo kutoka serikali ya China na ikikamilika ina uwezo wa kukalisha wasomi 2,600 kwa wakati mmoja.

Rais Magufuli amesema wanafunzi ambao walifukuzwa walistahili na asingefahamu hali hiyo ila baada ya wao kuanza kufanya migomo ikabidi wachunguzwe baada ya hapo ikabainika kwamba wapo pia watoto wa vigogo ambao walikuwa hawana sifa lakini walisajiliwa chuoni hapo.

Rais amesema kwa wanafunzi ambao wana Divison 1 na Division 2 watasaidiwa namna ya kuendelea na masomo ila kwa wenye Divison 3 na 4 waanze kutafuta kazi za kufanya au kwenda vyuo vyenye hadhi yao.

Aidha Rais Magufuli amesema anashangazwa sana na wanasiasa wanaowatetea wanafunzi hao na kusema kwamba mambo ambayo ni ya muhimu kwa taifa ni lazima yapewe kipaumbele na kuacha itikadi za kisiasa.