Ijumaa , 27th Mei , 2016

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema ataendelea na sera yake ya kupambana na rushwa na ufisadi mpaka mwisho bila kujali nafasi ya mtu kwa maendeleo ya Taifa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwahutubia Wakandarasi, Wahandisi na wadau mbalimbali wa sekta ya Ujenzi.

Akizungumza Jana jijini Dar es Salaam, wakati akifungua Mkutano wa mwaka wa makandarasi wa mkoa wa Dar es Salaam, Mbeya na Dodoma, Dkt. Magufuli amesema wakati anaingia madarakani kuna watu walifikiri atakua upande wao.

Dkt. Magufuli amesema kuwa kamwe hawezi kushirikiana na kwa kuwa nafasi aliyopewa kwa sasa amepewa na Mungu kwa ajili ya kuwatumia Watanzania ambao wengi wao ni masikini na kuongeza yupo tayari kurudi kuchunga Ng'ombe lakini sio kushirikiana nao.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, (TAKUKURU), Valentino Mlowola amesema kuwa Sekta ya Wakandarasi ndio inakabiliwa na changamoto ya rushwa hivyo washirikiane na taasisi hiyo kutoa taarifa pindi wanapopata taarifa hizo.

Nae Mwenyekiti wa Bodi ya Wakandarasi nchini, Mhandisi Consolata Ngimbwa, ametumia fursa hiyo kumshukuru rais Magufuli kwa kuanza kuwalipa Wakandarasi na kusema hali ya wakandarasi ilikuwa mbaya sana na sasa wameanza kuiona ahueni.

Sauti ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwahutubia Wakandarasi, Wahandisi na wadau mbalimbali wa sekta ya Ujenzi