Alhamisi , 16th Apr , 2015

Wakulima mkoani Morogoro waandamana kwa lengo la kuzuia ujenzi wa nyumba katika viwanja vyenye mgogoro

Zaidi ya wakulima 80 wa eneo la Mguluwandege na Lukobe kata ya Kihonda manispaa ya Morogoro wameandamana kwa lengo la kuhamishia makazi katika ofisi za ardhi manispaa ya Morogoro wakishinikiza mkurugenzi kutoa amri ya kuzuia ujenzi wa nyumba katika viwanja vyenye mgogoro hadi kesi ya msingi iliyoko mahakama kuu ya ardhi itakapotolewa uamuzi

Wakizungumza kwa uchungu huku wakiwa wamebeba masufuria ya kupikia pamoja na mikeka ya kulalia kambini hapo wakulima hao wameeleza kushangazwa na hatua ya halmashauri ya manispaa ya Morogoro kukaidi amri iliyotolewa na mahakama kuu ya ardhi na kukaziwa na waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi Wiliamu Lukuvi ya kuwataka kusimamisha ujenzi katika viwanja vyenye mgogoro kati ya wakulima hao na manispaa.

Mgogoro huo umedumu kwa miaka 10 sasa ingawa kesi ya msingi iko mahakamani lakini manispaa wanaendelea kuuza viwanja katika eneo hilo ambapo wamesema wanaweka kambi ofisini hapo hadi agizo hilo litakapo tekelezwa…

Mkuu wa wilaya ya Morogoro mjini Jordan Rugimbana amemwagiza mkurugenzi wa halmashauri ya manispaa ya Morogoro Bi Theresia Muhongo kuzuia utoaji wa viwanja unaoendelea na kusimamisha ujenzi kwa walio uziwa viwanja mpaka mahakama itakapotoa mamuuzi ya mgogoro huo.

Kufuatia kauli hizo za mkuu wa wilaya wananchi hao wameonekana kuridhika ambapo wamechukua mikeka yao masufuria, sahani na vikombe ambavyo walibeba kwa lengo la kuhamishia makazi katika ofisi ya ardhi mansipaa ya Morogoro.