Jumanne , 19th Aug , 2014

Wakulima mkoani Ruvuma nchini Tanzania wamelalamikia uongozi wa mkoa huo kwa kuchelewa kufungua soko kubwa la mahindi kama alivyoagiza Rais Jakaya Mrisho Kikwete wakati alipokuwa katika ziara ya mkoa huo na kuagiza kufunguliwa kwa soko hilo.

Rais wa Tanzania Dkt Jakaya Mrisho Kikwete.

Katibu mtendaji wa umoja wa wafanyabiashara wa mazao mkoani Ruvuma (UWAMARU) Bw. Tadei mwakaguo amehoji utekelezaji wa kauli ya Rais kuhusu kufungua soko la mazao na kuitaka serikali kutoa ufafanuzi.

Hata hivyo mkuu wa mkoa wa Ruvuma Mhe. Said Mwambungu amesema kuwa walikuwa wakisubiri kufungua vituo vya vijijini ambapo wameshafungua vituo vinne na kwamba suala hilo linahitaji michakato.

Michakato hiyo kwa mujibu wa mkuu wa mkoa Mwambungu ni pamoja na kuandaa magunia ya kuhifadhia mahindi na kutoa mahindi yaliyopo ili kuhifadhi mahindi mapya na kwamba kwa sasa michakato imekamilika hivyo yataanza kununuliwa muda wowote kuanzia wiki hii.

Katika hatua nyingine, wajasiriamali nchini Tanzania wanatarajiwa kupatiwa uwezo zaidi ili waweze kuzalisha bidhaa za viwango vya juu itakayowasaidia kukuza ushindani katika masoko ya kimataifa.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam Afisa mtendaji kutoka kampuni ya Food Safety and Quality Consultancy, Paul Seni amesema lengo ni kuwasaidia wajasiriamali wa Tanzania kufahamu kuhusu uandaaji wa ubora wa vyakula na kujumuisha matumizi ya mbolea, viwatilifu na namna ya kuondoa visumbufu vinavyoharibu ubora wa mazao tokea shambani.

Aidha, Bw Seni amesema kwa kulitambua hilo kampuni hiyo imedhamini makongamano katika mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza yanayotarajiwa kuanza tarehe 25 hadi 29 mwaka huu na kuwataka wajasiriamali kuhudhuria kwa wingi ili kupata uelewa huo.