Jumamosi , 27th Mei , 2017

Waumini wa dini ya kiislamu nchini wametakiwa kuutumia vizuri mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa kufanya matendo mema pamoja na kudumisha amani ndani ya taifa la Tanzania

Muft wa Tanzania, Sheikh Abubakary Zubery

 

Wito huo umetolewa na Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakary Zubeiry Ally wakati akizungumza na Hotmix ya EATV kuhusu kuanza kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan na kusema kuwa katika kipindi hiki waislamu wanapaswa kuwasaidia watu wasiokuwa na uwezo wakiwemo, yatima na watu wengine.

“Nchi ikikosa amani hata shughuli nyingine za maendeleo na ibada haziwezi kufanyika kama inavyopaswa, hivyo basi ni muhimu kwa waislamu nchini kuwa mfano wa kudumisha amani na upendo”. Alisema Mufti

Sheikh Zubery, ameongeza kuwa katika mwezi huo Mtukufu wa Ramadhan Waislamu wanatakiwa kuishi kwa mapenzi na upendo, ikiwa ni pamoja kuwangalia na kuwasaidia wale wasiokuwa na uwezo wakiwemo, mayatima na watu wengine wasiojiweza.

Katika hatua nyingine naye, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salum amewasihi waislamu kiujumla kuutumia mwezi mtukufu wa Ramadhan katika kuiombea nchi pamoja na kusameheana kwa waliokoseana bila ya kusahau kutoa misaada kwa watu wasiojiweza.