Alhamisi , 5th Feb , 2015

Hatimaye  wafugaji mkoani  Morogoro wamesitisha mgomo  na  kufungua minada ya mifugo  kufuatia serikali kuwahakikishia usalama baada ya kudhibiti madereva wa bodaboda waliokuwa  wakipigwa wafugaji kila wanapoingia katika  mji wa Morogoro.

Wakizungumza katika mkutano uliohusisha  wafugaji na uongozi wa serikali ya wilaya ya Morogoro wafugaji hao wamesema wameridhika na maelezo yaliyotolewa na serikali kuhusu kuchukua hatua dhidi ya madereva wa bodaboda waliokuwa wakiwavamia wafugaji.

Pia wamesema wanataka kuona hatua sahihi zikichukuliwa na kuona  fidia zinatolewa kwa  wafugaji walioathirika katika migogoro hiyo.

Naye  mkuu wa wilaya ya Morogoro Saidi Amanzi  amesema  atafikisha malalamiko ya wafugaji katika ngazi za juu lakini pia amewakumbusha kuanza kufikiria kupunguza mifugo  na kuanza  kuwekeza.

Mkuu wa polisi wa wilaya Zuberi Chembela amewatoa hofu  wafugaji  waendelee kufanya shughuli zao za maendeleo mjini Morogoro na kueleza hatua walizozichukua kwa madereva wa boda boda  waliobainika kuwapiga wafugaji mjini Morogoro.

Nje ya mkutano  wafugaji wamesema sasa imetosha kwa migogoro ya wakulima na wafugaji na kuomba dola kusimamia sheria za ardhi zilizopo kwa  kuheshimu mipaka ya kisheria katika vijiji vilivyotengwa kwa ajili ya wakulima na wafugaji ili kuondoa muingiliano  wa shughuli za kilimo na ufugaji