Jumamosi , 10th Jan , 2015

Wafugaji wa tarafa mbili za Mswaki na Mgera wilayani Kilindi wameiomba serikali kuharakisha zoezi la kuwapimia mipaka inayotenganisha kijiji kimoja kwenda kingine kufuatia baadhi ya viongozi wa serikali za vijiji kuendelea kuuza maeneo.

Sehemu ya jamii ya wafugaji wilayani Kilindi

Wafugaji wa tarafa mbili za Mswaki na Mgera wilayani Kilindi wameiomba serikali kuharakisha zoezi la kuwapimia mipaka inayotenganisha kijiji kimoja kwenda kingine kufuatia baadhi ya viongozi wa serikali za vijiji kuendelea kuuza maeneo yaliyotengwa kisheria kwa ajili ya wafugaji.

Hatua hiyo ilisababisha watu sita kuuawa kufuatia mapigano yaliyotokea kwa nyakati tofauti katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu.

Wakizungumza baada ya viongozi wa serikali ngazi ya tarafa ya Mswaki kuwaita wafugaji kujadili migogoro ya ardhi kufuatia waziri wa maendeleo ya mifugo na uvuvi Dkt Titus Kamani kuuagiza uongozi wa serikali ngazi ya mkoa na wilaya kulitafutia ufumbuzi suala hilo, wafugaji hao wamesema endapo serikali haitapima mipaka na kuweka mipango ya matumizi bora ya ardhi mapigano hayatakwisha.

Wamesema sababu kubwa ni idadi kubwa ya wageni kutoka mikoa ya Manyara na Arusha kuzidi kuongezeka na kupewa ardhi kinyume cha sheria kupitia kwa viongozi wa serikali za vijiji na kata.

Akielezea matukio ya vifo vilivyotokana na mapigano baina ya wafugaji, wakulima na wageni kutoka mikoa ya Manyara na Arusha waliouziwa maeneo kinyemela na viongozi wa serikali za vijiji, Kaimu Afisa Mtendaji wa serikali kata ya Msanja Mwanaidi Gwalu ametaja maeneo yenye migogoro iliyosababisha mapigano na watu kuuawa katika mazingira ya kutatanisha kuwa ni kijiji cha Muungano, Kwadudu na Mswaki na hadi hali bado ni mbaya katika kijiji cha Tingetinge

Hata hivyo katika kikao hicho kilichokutanisha viongozi wa serikali za vijiji husika, wafugaji na viongzoi wa jeshi la polisi, wafugaji walikisusia na kuamua kutoka nje kwa madai kuwa wanamtaka mkuu wa wilaya ambaye ndiye mlengwa wa kikao hicho na sio afisa tarafa.

Wamesema Afisa tarafa amechanganya vikao viwili vya kamati ya ulinzi na usalama ngazi ya tarafa huku baadhi ya watuhumiwa wakiwa ni miongoni mwa waalikwa waliouza mashamba ya wafugaji kwenye kikao hicho, hatua ambayo wafugaji waliamriwa kusalimisha silaha zao jadi nje ya ukumbi kwa kuhofia hali ya usalama kuwa tete