Jumatano , 28th Jun , 2017

Washiriki zaidi ya 2500 kutoka ndani na nje ya Afrika wamethibitisha kushiriki Maonesho ya 41 ya biashara ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba Julai 1 mwaka huu  yanayotarajiwa kufunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.John Magufuli.

Rais John Pombe Magufuli

Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, amesema Rais Magufuli atafanya ufunguzi huo katika Uwanja wa Maonesho wa Mwalimu Julius Nyerere uliopo barabara ya Kilwa Jijini Dar es Slaam.

Aidha, Waziri Mwijage amesema lengo la maonesho hayo ni kutoa fursa kwa wafanyabiashara wa ndani kujifunza mambo ya biashara na uzalishaji bora wa bidhaa kulingana na soko la kimataifa, kutengeneza mitandao ya mawasiliano baina yao ambayo itawasaidia kukuza biashara na kufikia malengo waliyojiwekeka, kutoa fursa ya kuuza bidhaa zao pamoja na kuruhusu taasisi  mbalimbali kutangaza biashara na huduma bila ya kuwasahu wafanyabiashara wa nje pia.

Picha kutoka Maktaba ikiwa inamuonesha Waziri Mwijage alipokuwa ametembelea banda la wanyama TANAPA

“Maonesho haya yanabeba kauli mbiu isemayo ukuzaji wa biashara kwa maendeleo ya viwanda, inalenga kutumia maonesho haya kama jukwaa la kutangaza biashara na huduma mbalimbali kwa ajili ya ukuzaji wa sekta ya viwanda, ikizingatiwa kuwa serikali ya awamu ya tano inaweka mkazo mkubwa katika kuendeleza uchumi wa viwanda hapa nchini” ilisema taarifa ya Waziri.

Pamoja na hayo, Mwijage amesema maonesho ya mwaka huu yatatoa fursa kwa wenye viwanda vidogo, vya kati na vikubwa kukutana na wanunuzi wa bidhaa zao pamoja na kuwepo na kampeni ya kuhamasisha wananchi kupenda kutumia bidhaa zilizozalishwa hapa nchini.

Mpaka sasa baadhi ya nchi ambazo zitakazoshiriki katika maonesho hayo ni pamoja na Burundi, China, Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Misri, Ujerumani, Ghana, India, Indonesia, Iran, Italia, Japan, Kenya, Malawi na Mauritius.