Alhamisi , 14th Jan , 2021

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, limewaagiza wabunge wote kuwasili jijini Dodoma, Januari 17, 2021, kwa ajili ya kuanza kwa vikao vya kamati za kudumu za Bunge zitakazoanza rasmi Januari 18 mwaka huu.

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taarifa hiyo imetolewa na kitengo cha mawasiliano na uhusiano wa kimataifa cha Bunge, na kueleza kuwa kamati zote za kudumu za Bunge zitafanya uchaguzi wa wenyeviti na makamu wenyeviti.

Aidha wajumbe wa kamati za kudumu za Bunge, watapewa mafunzo mbalimbali ikiwemo juu ya majukumu na taratibu za uendeshaji wa kila kamati, mafunzo kuhusu Bunge mtandao na usalama wa mitandao kwa kamati zote, pamoja na mafunzo kwa kamati za sheria ndogo kuhusu uchambuzi wa sheria ndogo na uzoefu wa mabunge mengine ya nchi zinazofuata mfumo wa kibunge wa jumuiya ya madola.

Mbali na mafunzo hayo pia kamati ya bajeti itapokea na kujadili mambo mbalimbali ikiwemo mapendekezo ya mpango wa maendeleo ya Taifa ya mwaka mmoja, mwongozo wa kuandaa mpango wa bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2021/2022, pia itajadili utekelezaji wa bajeti ya serikali pamoja na sheria ya fedha kwa kipindi cha nusu mwaka kwa mwaka wa fedha 2020/ 2021.