Jumapili , 14th Sep , 2014

Waathirika wa milipuko ya mabomu iliyotokea Aprili 29 mwaka 2009 huko Mbagala nje kidogo ya jijini Dar es Salaam, wamemuomba Rais Jakaya Kikwete kuwasaidia kupata stahiki zao zilizosalia.

Moja ya nyumba zilizoathirika na milipuko ya mabomu Mbagala mwaka 2009.

Stahiki hizo kwa mujibu wa wakazi hao ni nyongeza ya fedha kutokana na malipo waliyolipwa awali baada ya kufanyiwa tathimini ya uharibu wa nyumba zao kutoendana na uhalisia wa hasara kamili.

Wakizungumza kwenye mkutano wa pamoja uliofanyika Mbagala nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, Waathirika hao wamedai kulipwa fedha kidogo na kushindwa kujenga nyumba zao kama zilivyokuwa hapo awali huku wengine wakilalamikia kuishi kwenye mahema jambo ambalo wamesema limeathiri afya zao.

Waathirika hao wamesema kuwa kamati yao imefatilia ofisi mbalimbali za serikali kuhusiana na suala lao bila mafanikio na ndio maana wameamua kutumia vyombo vya habari ili kuweza kufikisha ujumbe wao huo.

Wakati huo huo, Waandishi wa habari nchini wameshauriwa kulinda usalama wa maisha yao katika kutimiza majukumu yao ya kila siku kwani hakuna habari iliyo na umuhimu kubwa kuliko thamani ya maisha yao.

Wito huo umetolewa na katibu mkuu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mkajanga, wakati akifunga mafunzo ya siku nne ya uandishi wa habari kwenye hali tete, mafunzo yaliyotolewa kwa waandishi wa habari mkoani Dodoma.

Amesema MCT imeamua kutoa mafunzo hayo kwa waandishi wa habari nchini Tanzania ili kuwawezesha kujilinda na kuchukua tahadhari ya maisha yao wakati wanapotekeleza majukumu yao, baada ya kubaini kuwa waandishi wengi nchini wanafanya kazi katika hali tete bila ya kujua jinsi ya kujikinga na mazingira hayo.