Jumanne , 26th Sep , 2017

Polisi nchini Kenya wamelazimika kutumia mabomu kuwatawanya kwa mabomu ya machozi wafuasi wa vyama vya Jubilee na muungano wa upinzani wa Nasa baada ya kuzua vurugu katika ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) zilizoko jengo la Anniversary Towers

Makundi hayo mawili yote yalikuwa yakiimba nyimbo tofauti ambapo kundi la Wafuasi wa Nasa waliokuwa wakiimba nyimbo “Chiloba lazima ang’oke” na upande wa Jubilee  Wafuasi wa Rais Uhuru walikuwa wakiimba 'Tunataka amani'

Aidha makundi hayo yote mawili yalitimua na kukimbilia mbali baada ya kukwepa kukamatwa na polisi wa kikosi cha kuzuia ghasia baada ya kuwarushia mabomu ya kutoa machozi.

Hata hivyo maandamano ya upande wa Nasa yamefanyika kuitikia wito uliotolewa jana na kiongozi mkuu Raila Odinga kwamba wafuasi wake wajitokeze kwa wingi kuandamana hadi kwenye makao makuu ya IEBC lengo likiwa kumtoa kwa nguvu Ofisa Mtendaji Mkuu wa IEBC, Ezra Chiloba kwa madai ya kuhusika kuvuruga uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 8.

Maandamano hayo yanafanyika siku chache baada ya Mahakama ya Juu kufuta ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta. Katika mji wa Kisumu, ambao unatajwa kuwa moja ya ngome za Nasa baadhi ya wakazi waliandamana hadi ofisi za IEBC na baada ya kufika walitoa wito maofisa wa ngazi za juu akiwemo Ezra Chiloba wajiuzulu.