Ijumaa , 25th Sep , 2020

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini John Shibuda amewataka wagombea wote kutoka vyama mbalimbali kuepuka kupandikiza chuki katika taifa ambapo ameviasa pia vyombo vya dola kusimama imara katika ulinzi wa tunu za Watanzania wakizingatia weledi.

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini John Shibuda.

Bw. Shibuda ambaye naye pia ni mgombea urais kupitia ADA-TADEA amsema kwamba mfumo wa vyama vingi nchini ni kichocheo cha maendeleo na si kuchochea mafarakano hivyo wagombea wa nafasi mbalimbali kutoka vyama mbalimbali vya siasa katika uchaguzi wa Oktoba 28 wazingatie weledi endapo watapatiwa ridhaa ya uongozi.

"Watanzania tukukumbe Tanzania hii itajengwa na sisi wenyewe tusisahau kuwa maumivu ya leo ni uimara wa kesho Viongozi watakaopata ridhaa ni muhimu kuzingatia utaifa kwanza", amesema John Shibuda.

Katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi amevitaka vyama vya siasa vijenge hoja na nasaha kwa Watanzania na kwamba uongo wa siasa huzaa dhuluma kwa vizazi ambavyo havitashiriki kupiga kura kwa kuwa ukweli huzaa haki.

Amesisitiza kuwa siasa ni kaa la moto ukilikanyaga bila kiatu lazima utaungua huku  akivitaka vyama vya Siasa 19, vilivyopata ridhaa kuwania nafasi ya Ubunge na Udiwani pamoja na vyama 15 vilivyopata ridhaa za wagombea wao kuwania nafasi ya Rais kutangaza sera zao kwa Watanzania ili wafanye maamuzi sahihi ifikapo siku ya kupiga kura Oktoba 28, 2020.