Jumapili , 21st Sep , 2014

Serikali imeshauriwa kuongeza vituo vya utabiri wa hali ya hewa hapa nchini ili kuwasaidia wananchi hasa wa vijijini katika kupanga shughuli mbalimbali za kimaendeleo, jambo litakalisaidia katika kuondoa hasara za mara kwa mara hasa kwa wakulima.

Naibu Waziri wa Uchukuzi nchini Tanzania, Dkt Charlez Tizeba.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dkt Charlez Tizeba, amesema hayo wakati akifungua mkutano wa wakuu wa mamlaka za hali ya hewa kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika – SADC, na kuongeza kuwa licha ya jitihada za mamlaka ya hali ya hewa nchini kutoa taarifa, bado kumekuwepo na changamoto ya watanzania wengi kushindwa kufuatilia taarifa hizo na hivyo kujikuta wakikumbwa na maafa.

Akizungumza katika mkutano huo wa SADC mkurugezi wa mamlaka ya hali ya hewa wa Tanzania Agness Kijazi, amesema mkutano huo utasaidia nchi wanachama katika kuweka mikakati itakayosaidia katika kutoa taarifa zitakazo kuwa na manufaa kwa jamii katika shughuli zao mbalimbali.

Wakati huo huo, Serikali ya Tanzania imetakiwa kushughulikia mapema tatizo la ajira kwa vijana ili kuepukana na athari inayoweza kutokea kama ilivyokuwa moja ya vyanzo vya machafuko katika nchi za Afrika zinazozungumza kiasrabu.

Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, ametoa wito huo wakati akifungua mkutano wa kujadili kampeni mbalimbali kwa vijana kutoka vyama rafiki vya upinzani katika nchi za Tanzania, Uganda na Kenya, vyama vinavyounda Umoja wa Demokrasia barani Afrika - DUA.

Kwa upande wao, washiriki wa mkutano huo wamezitaka mamalaka zinazohusika na uongozi katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kuwa makini na maswala ya katiba na ajira kwa vijana zaidi tofauti na hali ilivyo hivi sasa.