Ijumaa , 4th Mar , 2016

Viongozi wakuu wa nchi za EAC, wameelezea azma yao katika kuboresha maisha ya watu, kwa kuimarisha miundombinu ya mawasiliano ikiwemo barabara, na kufungua mipaka, hatua itakayorahisisha ufanisi katika bishara na kukuza uchumi wa Jumuiya.

Viongozi wakuu wa nchi za EAC

Marais John Magufuli wa Tanzania,Yoweri Museven wa Uganda,Dakta Ally Mohamed Shein wa Zanzibar na Makamu wa Rais kutoka nchi za Burundi na Sudan kusini pamoja na mwakilishi wa Rais wa Rwanda Paul Kagame kwa pamoja wameonesha kukerwa na umasikini wa wananchi wa ukanda huu.

Katika uwekwaji wa Jiwe la Msingi la ukarabati wa Barabara ya kutoka Arusha-Holili-Taveta-Voi zoezi lililofanyika katika eneo la Tengeru Arusha,hotuba za wakuu wa mataifa ya Afrika Mashariki zimelekeza hatua muhimu katika kufikia uboreshwaji wa huduma za kijamii kwa wana Afrika Mashariki.

Awali Marais Yoweri Museven wa Uganda pamoja naye Rais Uhuru Kenyata wa Kenya wameelezea umuhimu wa Afrika Mashariki kuamka na kuboresha miundombinu ya kisekta pamoja na kuondolewa kwa vikwazo vyote mipakani na kurahisisha watu kuvuka nchi moja hadi nyingine.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dakta John Pombe magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya amesema ujenzi wa barabara hiyo ni ushahidi kwamba umoja uliopo ndani ya Jumuiya ni mwanzo wa kuhakikisha nchi zote za ukanda huu zinaunganishwa kwa njia ya barabara ambazo zitakuwa chachu ya maendeleo kwa wananchi.

Mapema kabla ya hotuba za viongozi hao wawakilishi kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika Gabriel Negatu pamoja naye balozi wa Japan Nchini Tanzania Masaharu Yoshida wamesema miradi ya aina hiyo ni muhimu kwa wana Afrika Masariki.

Barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 234.3, inayojengwa na mkandarasi Hanil-jiangsu itagharimu kiasi cha shilingi bilioni mia mbili na tisa ambapo bilioni mia moja na tisini ni fedha za mkopo kutoka benki ya maendeleo ya Afrika AfDB na kiasi kinachobaki bilioni kumi na tisa kimetolewa na nchi wanachama.

Zoezi hilo linahitimisha uwepo wa viongozi hao Jijini Arusha ambapo kabla ya hapo walishiriki mkutano wa 17 wa kawaida wa wakuu wa nchi hizo ambapo pamoja na mambo mengine waliipitisha nchi ya sudani kusini kuwa mwanachama mpya wa EAC.