Jumatatu , 21st Jul , 2014

Miradi ya maji na umeme katika baadhi ya maeneo ya halmashauri ya wilaya ya Chemba imeshindwa kutekelezeka kutokana na imani za kishirikina ambapo wakandarasi wa umeme wamekuwa wakikumbana na nyoka kila wanapochimba kusimika nguzo za umeme.

Baadhi ya wakazi katika wilaya ya Chemba wakitafuta maji

Miradi ya maji na umeme katika baadhi ya maeneo ya halmashauri ya wilaya ya Chemba imeshindwa kutekelezeka kutokana na imani za kishirikina ambapo wakandarasi wa umeme wamekuwa wakikumbana na nyoka kila wanapochimba mashimo ya kusimika nguzo, na kwenye miradi ya maji mabomba yanapasuka muda mfupi baada ya kufukiwa ardhini kwa madai ya wakandarasi hao kutowashirikisha wazee wa kimila kabla ya kuanza kwa miradi hiyo.

Changamoto hiyo ya kushangaza kama sio ya kustaajabisha imeibuliwa na mwenyekiti wa halmashauri hiyo mpya Muheshimiwa Rajabu kwenye zoezi la kutia saini mikataba ya ujenzi wa mifumo wa usambazaji maji katika vijiji vitano vya wilaya hiyo ambapo ametoa taadhari kwa wakandarasi watakaotekeleza miradi hiyo kuacha kuchelea kuwaona wazee wa vijiji hivyo ili kuepuka matukio kama hayo kuendelea kujitokeza na kuchelewesha maendeleo kwa wananachi.

Kaimu mhandisi wa maji wawilaya ya Chemba Robert Mganga amethibitisha kuwepo kwa matukio ya aina hiyo na kudai kuwa yamekuwa yakikwamisha utekelezaji wa miradi huku mhandisi kutoka wakala wa umeme vijijini (REA) Onesmo Kilamuhama akidai kuwa wamekuwa wakilazimika kufanya matambiko mara kwa mara na wazee wa kimila ili kupata ridhaa ya kutekeleza mradi huo.

Awali katika zoezi hilo mkuu wa wilaya ya Chemba Francis Isaac Mtinga amesema uhaba wa maji ni changamoto kubwa inayowakabili wakazi wa wilaya hiyo ambapo asilimia 66 hawapati maji kabisa  hali inayochangiwa na kushindwa kushiriki katika shughuli za maendeleo, huku wakikabiliwa na magonjwa yakiwemo ya ngozi, homa ya matumbo na kuhara mara kwa mara.

Ujenzi wa mfumo wa usambazaji maji katika vijiji vitano vya wilaya hiyo kupitia mpango wa serikali wa matokeo makubwa sasa utagharimu kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 1.187 ambao unatarajiwa kupunguza adha ya maji na wananchi kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma hiyo huku wakishindwa kushiriki katika shughuli za maendeleo