Urithi wa Mkapa kwa Watanzania

Alhamisi , 31st Dec , 2020

Usiku wa kuamkia Julai 24, 2020, Tanzania ilipata pigo kubwa baada ya kuondokewa na Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin William Mkapa, aliyefariki dunia katika moja ya hospitali zilizopo ndani ya jiji la Dar es Salaam, taarifa ambazo zilitolewa na Rais Dkt. John Magufuli.

Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin William Mkapa, wakati wa uhai wake.

Tanzania ilizizima, mataifa mbalimbali Duniani yaliomboleza na Taifa hili, haikuwa jambo rahisi kwa Rais Dkt. John Magufuli, kutangaza taarifa za kifo cha mtangulizi wake huyo katika madaraka, lakini ombi lake kwa Watanzania lilikuwa ni moja tu kuwa waendelee kuwa watulivu na wamoja katika kipindi hicho cha majonzi makubwa.

Huo ulikuwa ni msiba mwingine mkubwa wa kitaifa baada ya ule wa aliyekuwa Rais wa kwanza wa Tanzania Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambao ulitokea Oktoba 14, 1999, na katika kipindi chote cha maombolezo bendera zote zilipepea nusu mlingoti.

Rais Mkapa, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 81, na kuzikwa kijijini kwao Lupaso, Masasi mkoani Mtwara, ikumbukwe tu alifariki ikiwa imepita miezi takribani nane, tangu alipozindua kitabu chake alichokipa jina la "My Life My Purpose", ambacho kilizinduliwa katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) na Rais Dkt. Magufuli na kuhudhuriwa na marais wengine wastaafu Dkt. Jakaya Kikwete, Mzee Ali Hassan Mwinyi na viongozi wengine.

Mkapa ambaye alizaliwa mwaka 1938 mjini Ndanda, alihitimu shahada yake ya kwanza katika Chuo Kikuu Cha Makerere nchini Uganda na baadaye Chuo Kikuu cha Columbia, ambapo alipata shahada ya uzamili katika taalumu ya mahusiano ya umma, alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia mwaka 1995  hadi 2005.

Wakati wa uhai wake amewahi kupata nyadhifa mbalimbali katika ngazi ya mikoa na serikali ya Tanzania zikiwemo Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu, Wizara ya Mambo ya Nje na katika utawala wake kama Rais, pamoja na masuala mengine ya jitihada za upatanishi atakumbukwa na hatua za ubinafsishaji wa mashirika ya umma nchini.