Jumamosi , 23rd Sep , 2017

Nchi ya Tanzania imetakiwa kujifunza madhara ya uvunjifu wa amani na machafuko yaliyowahi kuzikumba nchi jirani zinazoizunguka ambao hadi leo wamshindwa kufikia kiwango cha kuitwa nchi yenye amani kama ilivyo Tanzania.

Akizungumza na hadhara iliyohudhuria maadhimisho ya siku ya amani Duniani yaliyo andaliwa na umoja wa mataifa UN Tanzania kamishna wa polisi jamii nchini CP Musa Ali Juma amesema uwepo wa makambi ya wakimbizi nchini ni ishara yakuwa uvunjifu wa amani ni adui wa ustawi wa jamii na maendeleo ya taifa

“Nawaomba watu waelewe kwamba kukosa amani sio jambo nzuri na si kitu cha kutamani hata siku moja kitokee, yapo madhara makubwa yanatokea kama tukiwa hatuna amani na waathirika wakuu wa jambo hilo ni wakinamama na watoto ambao kwa kiasi kikubwa madhara wanayoyapata hubakia kwa muda mrefu” amesema

Musa amesema maendeleo ya nchi yoyote katika nyanja ya kiuchumi na kijamii yanategemea amani hivyo kila mtanzania anawajibu wa kuitunza ili yasije yakatokea mambo machafu na vita kama ambavyo vinatokea katika nchi zingine barani Afrika na Duniani kwa ujumla.

"Taifa letu linawategemea vijana kwa maendeleo ya taifa hili hivyo wanapaswa kukumbuka kwamba wanajukumu kubwa la kulinda amani iliyopo tukishindwa kuidumisha amani iliyopo tujue kwamba maisha ya familia zetu yatakuwa hatarini hata maendeleo ya nchi na mtu binafsi yatakwama na yatakuwa ndoto,” ameongeza.

Aidha alisema walimu kwa nafasi yao wanawajibu wa kutoa elimu bora itakayomjenga mtoto ili baadae awe raia mwema mwenye kutunza amani iliyopo nchini.

“Sisi majeshi ya Polisi na mengine tuna kazi ya kusimamia na kuona kila mmoja katika jamii zetu anawajibika  kutunza amani na hawi kisababishi cha kuondoa amani, ndio maana anapojitokeza mtu anataka kuivuruga anashughulikiwa haraka,” alisema.

Aidha upande wa Ofisa Uhusiano wa UN, Stella Vuzo amesema  katika kuadhimisha amani hapa nchini UN inawahimiza viongozi wa Serikali kuhakikisha wanailinda na kuisimamia amani, ulinzi na usalama ili kuendeleza utulivu uliyopo.

“Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres alipokuwa akihutubia Baraza la Kimataifa la Amani duniani alisema uwepo wa amani katika nchi ni msingi wa maendeleo, siku hiyo katika bustani ya amani iliyopo makao makuu wa umoja huo New York nchini Marekani  aligonga kengere ya kuashiria amani na akahimiza mataifa yote kuitunza,” alisema.

Kwa upande wake Kiongozi Mkuu wa Kiroho wa Waislamu wa dhehebu la Shia Tanzania, Sheikh Hemed Jalala alisema misingi ya madhehebu ya dini duniani kote ni kuhimiza amani  hivyo wao kama viongozi ni wajibu wao kuendelea kuhimiza jambo hilo.