Jumamosi , 6th Feb , 2021

Wananchi wa kata ya Ifumbo wilayani Chunya mkoani Mbeya, wameripotiwa kuugua ugonjwa usiofahamika ambao mtu akiugua anatapika damu mpaka anapoteza maisha, na mpaka sasa tayari watu zaidi ya 15 wamefariki dunia na wengine zaidi ya 50 wanaendelea kuugua.

Diwani wa Kata ya Ifumbo, Weston Mpyila

Taarifa ya kuwepo kwa ugonjwa huo usiofahamika imeibuliwa na Diwani wa Kata ya Ifumbo, Weston Mpyila, mbele ya kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Chunya huku akiomba msaada wa kuwanusuru wananchi wake.

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya chunya, Ramadhan Shumbi, ameeleza hatua ambazo zimeshachukuliwa na halmashauri yake kukabiliana na ugonjwa huo huku wakiomba kuomba msaada wa kitaalam katika ngazi za juu ili kuubaini na hatimaye kupata tiba yake.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa wilaya ya Chunya, Dk. Felister Kisandu, amethibitisha kuwepo kwa ugonjwa huo ambao wameshindwa kuutambua na kudai kuwa ofisi yake imeomba msaada katika ngazi za juu ili wasaidiwe kuutambua na kukabiliana nao.