Jumatano , 13th Jan , 2021

Uganda imeagiza watoaji huduma za mtandao kufunga mitandao yote ya kijamii na programu za kutuma ujumbe kufikia Jumanne hadi wakati usiojulikana, kwa mujibu wa barua kutoka kwa mdhibiti wa mawasiliano nchini humo iliyonukuliwa na shirika la habari la Reuters.

Nembo za mitandao mbalimbali ya kijamii

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amethibitisha kufungiwa kwa mitandao hiyo katika hotuba yake ya jumanne usiku kabla ya muda wa mwisho wa kufanya kampeni, ambapo amesema ameagiza kufungwa kwa mtandao wa kijamii wa Facebook kwa kupendelea upande mmoja.

Rais Museveni ametuhumu mtandao wa Facebook kwenda kinyume na serikali ya nchi yake nakusema kuwa mtandao huo hauna mamlaka yakuhoji jambo lipi ni zuri au ubaya kwa nchi ya Uganda huku akisema kuwa endapo Facebook itatumiwa nchini Uganda, lazima itumiwe kwa usawa.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni

Kusitishwa kwa huduma kuna kuja katika kipindi ambapo nchi inajiandaa kwa ajili ya upigaji kura ndani ya wiki hii ilihali siku chache zilizopita mtandao wa kijamii wa Facebook ulifunga akaunti mbili za wanachama wa NRM (National Resistance Movement ) kwa kile kilichodaiwa kuwa matumizi mabaya ya akaunti hizo.

Awali  siku ya jumanne watumiaji walilalamika kwamba hawawezi kupata mtandao wa Facebook na WhatsApp, majukwaa ya mitandao ya kijamii inayotumiwa sana katika kipindi cha kampeni kabla ya uchaguzi wa urais kwenye nchi hiyo ya Afrika Mashariki.