Uchaguzi Mkuu, anguko kwa wapinzani

Alhamisi , 31st Dec , 2020

Oktoba 28, 2020, Tanzania iliingia kwenye joto la uchaguzi, kwa wananchi wake kuwachagua viongozi wao wanaowataka kwa nafasi za kiti cha urais, ubunge, udiwani na wawakilishi kwa upande wa Zanzibar, ambapo kwa mujibu wa viongozi wa serikali walisema kuwa uchaguzi huo ulifanyiaka kwa amani.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe.

Mara baada ya zoezi kukamilika saa 10:00 jioni, zoezi la uhesabuji wa kura ukaanza na baada ya kila jimbo kukamilisha kuhesabu kura lilitangaza washindi wa kiti cha ubunge, na matokeo ya mshindi wa ubunge ya kwanza kabisa kutangazwa yalikuwa ni yale ya jimbo la Hai mkoani Kilimanjaro.

Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, alimtangaza mshindi katika kinyang'anyiro hicho kuwa ni Saasisha Mafue wa Chama cha Mapinduzi (CCM), na kumuangusha aliyekuwa mbunge wa muda mrefu wa jimbo hilo kupitia CHADEMA Freeman Mbowe.

Kuangushwa kwa Mbowe katika kinyang'anyiro, kilileta minong'ono mingi kwa wananchi na wapenzi wa chama hicho, huku wengine wakidai kuwa kuangushwa kwake, huenda ikawa ni anguko kwa wabunge wote wa vyama vya upinzani, jambo ambalo lilileta uhalisia mkubwa kwani matokeo yote yaliyofuata yalionesha kuwa CCM ndiyo wanaoongoza.

Kama misemo ya waswahili isemavyo hohehahe hakosi siku yake, ndivyo ilivyotokea kwa chama kikuu cha upinzania nchini Tanzania cha CHADEMA, kwani kiliambulia walau kiti kimoja cha mshindi wa ubunge kupitia chama hicho ambaye ni Aida Khenani, kutoka jimbo la Nkasi Kaskazini.

Katika upande wa matokeo ya urais, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ilimtangaza pia Dkt. John Magufuli wa CCM, kuwa ndiye mshindi wa kiti hicho, akimshinda mpinzani wake kupitia CHADEMA Tundu Lissu.

Anguko katika uchaguzi mkuu, halikuwa kwa CHADEMA tu bali kwa vyama vingine kama ACT Wazalendo, NCCR-Mageuzi na CUF ambao nao waliambulia kiti kimoja cha ubunge.