Ijumaa , 12th Feb , 2016

Kesi inayomkabili Naibu Rais wa Kenya William Ruto katika Mahakama ya Kimataifa ya jinai (ICC) inatarajiwa kuchukua mwelekeo mpya leo, wakati kitengo cha rufaa kitakapotoa uamuzi juu ya taarifa za mashahidi watano waliojiondoa kama zitaendelea au la

Naibu Rais wa Kenya William Ruto akiwa Mahakamani The Huge nchini Uholanzi

William Ruto na mwanahabari Joshua Arap Sang walikata rufaa dhidi ya utumiaji wa taarifa hizo, baada ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) Fatou Bensouda kufanikiwa kushawishi majaji wanaosikiliza kesi yao kuruhusu zitumiwe.

Kwa mujibu wa na Bensouda, ushahidi huo ni muhimu kwenye kesi yake kwa kuwa mashahidi walikuwa wameeleza jinsi walivyohudhuria mikutano ambapo inadaiwa Ruto alitoa ufadhili wa kifedha na silaha kwa vijana waliotekeleza mashambulio dhidi ya wapinzani wa chama cha ODM baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2007.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, iwapo majaji wa rufaa watabatilisha uamuzi uliopelekea kutumiwa kwa taarifa hizo, itakuwa afueni kwa Ruto kwani anaamini ushahidi mwingine uliopo hautoshi kufanya ahukumiwe.

Kwa upande mwingine, majaji wa rufaa wakiamua kuwa uamuzi huo ulitolewa kwa njia inayostahili kisheria, itakuwa pigo kwa Naibu Rais huyo wa Kenya hasa kwa kuzingatia jinsi Bi Bensouda amekuwa akisisitiza kuwa mashahidi hao ndiyo mashahidi muhimu zaidi kwenye kesi yake.

Umoja wa Afrika na baadhi ya nchi zimekuwa zikiituhumu ICC kuwa ina upendeleo katika ufuatiliaji wa watuhumiwa kutokana na kuwaandama zaidi viongozi wa Kiafrika, tuhuma ambazo zinakanushwa na Mkuu wa Mashtaka wa mahakama hiyo Fatou Bensouda.