Jumatatu , 4th Apr , 2016

Wakulima na wadau wengine wa zao la Korosho wametakiwa kutilia mkazo kuuza korosho zilizobanguliwa ili kulipa hadhi zao hilo na kudhibiti wanunuzi holela wa mitaani maarufu kama Kangomba.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Halima Dendego

Akizungumza na East Africa Radio, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, amesema serikali ya Mkoa inajitahidi kupambana na mfumo huo wa ununuzi kwa kiasi kikubwa na kukiri kuwa bado kuna changamoto kubwa kuweza kuutokomeza.

Bi. Halima ameongeza kuwa Mfumo wa Kangomba unapaswa kutokomezwa haraka iwezekanavyo kwa kuwa unamfanya mkulima awe nyonge siku zote hivyo amesema mfumo wa sasa wa kubangua korosho utapunguza kwa kiasi kikubwa ununua holela wa zao hilo.

Aidha, amesema katika msimu huu uliomalizika ilijitokeza kangomba nyingine ambayo ilikuwa mbaya zaidi ambayo ni ya vyama vya msingi vilivyokuwa vikikusanya korosho kwa bei ya chini na kwenda kuziuza kwa bei ya juu katika minada.

Mkuu huyo wa Mkoa amesema tayari wameshaanza kulishughulikia suala hilo kwa kukusanya taarifa za viongozi wa vyama vya msingi waliojihusisha na ununuzi wa korosho kwa njia ya Kangoma na kusema wakibainika hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

Sauti ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Halima Dendego akizungumzia biashara holela ya Korosho"Kangomba"