Jumatano , 20th Mei , 2015

Serikali kupitia wizara ya fedha imesema imekwishapeleka fedha za mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kwenye taasisi husika na kuwataka viongozi waliopewa jukumu la kupeleka vyuoni pesa hizo kuzifikisha haraka ili kutatua tatizo hilo.

Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Mwigulu Nchemba akisisitiza jambo Bungeni

Akizungumza kwa niaba ya serikali leo Bungeni mjini Dodoma, Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Mwigulu Nchemba amekiri ucheleweshwaji wa fedha hizo na kutaka wahusika watoe kwanza fedha hizo kwa utaratibu wa dharura na sio kufuata mlolongo wa vikao uliozoeleka.

Mh. Mwigulu amesema kuwa serikali imeandaa mpango ambao utazifikisha fedha za mifuko rasmi pindi zitapokusanywa na kuacha utaratibu wa sasa ambao unaonekana unasababisha ucheleweshwaji wa utoaji fedha kwa taasisisi hizo ikiwemo mikopo ya wanafunzi.

Mwigulu ameongeza kuwa kwa niaba ya serikali wanawaomba radhi wanafunzi waliopata usumbufu kutokana ucheleweshwaji huo wa fedha na kuwataka wanafunzi hao warejee madarasani kwa kuwa tatizo lao limeshaanza kushughulikiwa.

Mwigulu alikuwa anajibu swali la Mbunge wa viti maalumu Dodoma aliyetaka muongozo wa spika kuwa serikali imechukua hatua gani baada ya wanafunzi wa chuo kikuu cha Dar es slaam kugoma kutokana na kucheleweshewa pesa zao.