Jumanne , 10th Mei , 2016

Serikali kupitia Benki ya Uwekezaji Tanzania-TIB, na Benki ya Maendeleo ya Kilimo-TADB, zimetoa mikopo yenye thamani za shilingi trilioni 1.106 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii na kimkakati ili kusaidia kukuza uchumi wa nchi.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji.

Akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Mhe. Innocent Bashungwa, aliyetaka kujua mchango wa taasisi hizo katika kukuza uchumi wa nchi, leo Mei 9, 2016, Bungeni Mjini Dodoma, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, alisema kuwa fedha hizo zimetolewa ili kufungua fursa za kiuchumi na kupunguza umasikini nchini.

Alitaja miradi iliyonufaika na mikopo hiyo ya muda wa kati na muda mrefu kuwa ni pamoja na Mradi wa Maendeleo ya Makazi katika wilaya za Temeke na Kinondoni, Jijini Dar es Salaam, Mradi wa Maendeleo ya Miji kupitia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Miradi mingine ni viwanda vya kubangua korosho, ujenzi wa maghala, mabomba ya maji, viwanda vya sukari na kilimo cha miwa, kukoboa na kusindika kahawa, matunda, mifuko ya hifadhi ya mazao na nyaya za umeme.

"Hadi mwaka jana, 2015, Benki ya Uwekezaji (TIB) imewawezesha watanzania wengi kupambana na umasikini kwa kutoa mkopo wa zaidi ya shilingi 550bn katika sekta mbalimbali za kiuchumi", alisema Dkt Kijaji.

Alisema kuwa Benki hiyo kupitia dirisha la kilimo, imetoa mkopo wa shilingi 58.8bn kuendeleza sekta ya kilimo kupitia kampuni binafsi 121, taasisi ndogondogo za fedha 11 na vyama vya akiba na mikopo SACCOs zipatazo 78.

"TIB imetoa mkopo wa shilingi 489.2bn kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 181 ya kusambaza umeme vijijini kupitia REA, ambapo Kaya 257,000 zimenufaika na mradi huo," alisisitiza Dkt. Kijaji.

Alibainisha kuwa vikundi 17 vya wachimbaji wadogo wadogo wa madini vimepatiwa mikopo yenye thamani ya shilingi 8bn kwa ajili ya kuendeleza sekta hiyo

Naibu Waziri huyo wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, alieleza kuwa mikopo hiyo imechangia kuongezeka kwa uzalishaji wa bidhaa zinazouzwa nje kamavile maua, kahawa na dhahabu.

"Pamoja na kwamba Benki ya Maendeleo ya Kilimo-TADB, haijaanza rasmi kutoa mikopo, TIB imejielekeza kwenye utekelezaji wa Ilani ya CCM na mipango mikakati mbalimbali ya maendeleo ya Taifa" Aliongeza Dkt. Kijaji

Katika hatua nyingine, Dkt. Kijaji aliliambia Bunge mjini Dodoma, kuwa serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, itafanya utafiti ili kujiridhisha juu ya umuhimu wa kujenga ofisi za taasisi hiyo katika wilaya ya Kilindi na nyinginezo nchini kwa kuzingatia gharama za usimamizi na fursa za mapato ya kodi katika maeneo husika. "Mpango uliopo sasa ni ujenzi wa ofisi za TRA katika makao ya mikoa mipya iliyoanzishwa nchini," aliongeza Dkt. Kijaji.

Aliwataka wananchi wa wilaya ya Kilindi na watanzania wote kwa ujumla kuendelea kulipa kodi kwa hiari na kwa mujibu wa sheria, ili fedha hizo zitumike kwaajili ya maendeleo ya Taifa.

Dkt. Kijaji, alikuwa akijibu swali la Mhe. Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi aliyetaka kujua mkakati wa serikali kujenga ofisi za TRA katika wilaya ya Kilindi ili kuwaondolea adha wananchi wake kwenda kulipa kodi kwenye wilaya nyingine ya Handeni, zilipo Ofisi za TRA.

Sauti ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji,