Alhamisi , 10th Sep , 2020

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewahimiza wamiliki wa majengo yaliyopimwa na ambayo hayajapimwa kulipia kodi stahiki za majengo wakiwemo wote wenye madeni kufanya hivyo ili kuepuka usumbufu wa kimfumo pindi wanaporundikana kwa kulipia kwa pamoja.

Mkurugenzi wa kitengo cha elimu kwa mlipa Kodi bw Richard Kayombo.

Akizungumza katika mahojiano maalum na EATV Mkurugenzi wa kitengo cha elimu kwa mlipa kodi Bw Richard Kayombo amesema kufanya hivyo ni sehemu ya wananchi kutimiza wajibu hasa katika robo hii ya kwanza.

"Kwa kawaida wamiliki wote wa majengo yanatakiwa kulipiwa kodi ikiwa imepimwa au haijapimwa na ni vyema wananchi wanafanya hivyo kwa maana zile siku za mwisho huwa zina changamoto kubwa zinazopelekea mifumo kuzidiwa."alisema Kayombo

Amesema kwa sasa mamlaka hiyo inaendelea na mpango wake wa kutembelea mlango kwa mlango kutoa elimu ya kodi lakini pia kuzifahamu changamoto za wafanyabiashara moja kwa moja.

"Hili zoezi tayari tunaanza kulitekeleza kwa mikoa ya Arusha,Mtwara,Kagera,Tabora, na kwa Dar es salaam tufanya katika Wilaya ya Ubungo tuu lengo ikiwa tunataka kila mwananchi apate uelewa kuhusu masuala ya kodi." alisema Kayombo.

Aidha Bw Kayombo amewataka waajiriwa kuhakikisha wanakabidhi utambulisho wa mlipa kodi (TIN) kwa waajiri wao zoezi ambalo limeongezwa hadi mwezi disemba 2020 ambapo wahusika watafanya maombi haya kwa njia ya kimtandao.