Jumatatu , 23rd Mar , 2015

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Tanzania imesema mvua zinazoendelea kunyesha nchini hivi sasa ni za kawaida kwa msimu wa masika na kwamba kuna haja ya wananchi kuendelea kufuatilia taarifa za utabiri wa hali ya hewa.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Tanzania, Dkt Agnes Kijazi.

Mkurugenzi wa mamlaka hiyo Dkt Agnes Kijazi, amesema hayo leo wakati akitangaza maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Hali ya Hewa na kuonya kuwa kuna wakati mvua hizo zinaweza kunyesha juu ya wastani na kuleta madhara.

Kwa mujibu wa Bi. Kijazi, wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari katika kipindi chote cha masika ambacho kinatarajia kufika hadi mwezi Mei mwaka huu na kwamba moja ya tahadhari hizo ni kutoishi maeneo ya bondeni ambayo ni maarufu kwa mafuriko pamoja na watumiaji wa bahari hususani wavuvi.

Bi. Kijazi amezitaja tahadhari nyingine ni za kutunza mazingira dhidi ya uwezekano wa kuibuka kwa magonjwa ya mlipuko pamoja na tabia ya wananchi kujiwekea akiba ya chakula ili pindi mazao yao yanapoharibiwa na mvua waweze kuwa na chakula cha akiba.

Mkurugenzi huyo wa mamlaka ya hali ya hewa ametaja mikoa ambayo itapata mvua kubwa katika kipindi hicho kuwa ni ile iliyo katika ukanda wa pwani ikiwemo mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Dar es Salaam, Unguja, Pemba pamoja na mkoa wa Tanga.