Jumanne , 30th Dec , 2014

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini TMA imetoa tahadhari ya uwezekano wa kuwepo kwa mvua za mfululizo pamoja na hali ya joto iliyo juu ya wastani kwa kipindi cha miezi miwili ijayo.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Tanzania TMA Dkt Agnes Kijazi

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Tanzania TMA Dkt Agnes Kijazi amesema kuwa viashiria vya hali ya hewa na joto vinaonesha kuwa maeneo mbalimbali nchini yataendelea kuwa na joto la juu ya wastani katika kipindi cha mwezi Januari hadi Februari 2015.

Hali ya ongezeko la joto pia inatarajiwa katika maeneo ya Magharibi na Kusini Magharibi mwa nchi ambayo mpaka sasa yamekuwa na joto la wastani.

Wananchi katika maeneo husika wameshauriwa kuchukua hatua stahiki kujikinga na athari za kiafya na mazingira zinazoweza kusababishwa na ongezeko la joto linaloendelea

Dkt Kijazi ameongeza kuwa wananchi wazingatie kuwa pamoja na kuwapo kwa matukio mengi ya mvua kubwa katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua juu ya wastani, hali hiyo pia inaweza kujitokeza katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani.

Amesema kuwa matukio ya vimbunga katika eneo la Kusini Magharibi mwa bahari ya Hindi yatarajiwa kuchangia katika mwenendo wa mvua nchini.

Ametaja maeneo ambayo hali ya mvua inaweza kuathiriwa zaidi na vimbunga kuwa ni pamoja na Kanda ya Kati, Nyanda za juu Kusini Magharibi, Magharibi mwa nchi na maeneo ya ukanda wa Pwani.