Ijumaa , 13th Jan , 2017

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa ameunda timu ya watu 12 kwa ajili ya kufanya uchunguzi kubaini chanzo cha tukio la kuwaka moto kwa sehemu ya kuhifadhi mizigo katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere DSM

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Profesa Makame Mnyaa Mbarawa akitembelea sehemu mbalimbali za Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam

 

 

Prof. Mbarawa amechukua hatua hiyo hii leo Jijini Dar es Salaam sambamba na kutoa muda wa mwezi mmoja kwa timu hiyo, baada ya kutembelea na kuona uharibifu uliosababishwa na tukio hilo lililotokea jana majira ya saa tano usiku na kuunguza kabisa shehena ya mizigo iliyokuwa katika chumba hicho kabla ya moto huo kuzimwa.

Sehemu hiyo ya kuhifadhia mizigo ipo chini ya kampuni inayotoa huduma za mizigo na usafiri uwanjani ya Swissport na kwamba mizigo hiyo ni ile ambayo aidha ilichelewa njiani au kusahaulika na ambayo ilikuwa njiani kuja kuchukuliwa na wamiliki wake.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini (TCAA), Bw. Hamza Johari ametaja hatua zilizochukuliwa baada ya moto huo kuzuka na kwamba kwa ujumla hatua hizo zimesaidia kuzuia uwezekano wa kutokea janga kubwa na kwamba kwa sasa huduma za usafiri uwanjani hapo zinaendelea kama kawaida.

Amesema kimsingi mamlaka yake ilitoa maagizo kwa waendeshaji wa uwanja huo, maagizo ambayo vyombo vya usalama ikiwemo kitengo cha zima moto kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kuuzima moto huo sambamba na kuhakikisha huduma za usafiiri hazitetereki.