Jumapili , 23rd Nov , 2014

Serikali imeamua kuunda timu ya watu 10 kutoka kada tofauti wakiwemo viongozi wa dini ambao watapewa jukumu la kufanya kazi ya usuluhishi kwenye vijiji vyenye migogoro baina ya wafugaji na wakulima wilayani Kiteto mkoani Manyara.

Serikali imeamua kuunda timu ya watu 10 kutoka kada tofauti wakiwemo viongozi wa dini ambao watapewa jukumu la kufanya kazi ya usuluhishi kwenye vijiji vyenye migogoro baina ya wafugaji na wakulima wilayani Kiteto mkoani Manyara.

Kauli hiyo imetolewa na waziri mkuu wa Tanzania Mh. Mizengo Pinda kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete wakati akiwasilisha salamu za Serikali kwenye ibada ya kumweka wakfu Askofu wa Sita wa Dayosisi ya Central Tanganyika ya Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Dickson Chilongani iliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu, mjini Dodoma.

Amesema “Hali ya Kiteto ni changamoto kama alivyosema Askofu Mkuu, Dk. Chimeledya lakini inahitaji ufumbuzi kutoka kwa wadau tofauti na siyo Serikali peke yake.

Ameongeza kuwa suluhu inataka Serikali, wananchi, vyombo vya dola lakini pia na Kanisa lazima lihusishwe ili kujenga upya maadili ya jamii.

“Ukiwa na kundi kubwa la watu ambao hawamwogopi Mungu ni tatizo, na hii ndiyo iliyoko kule. Watu wanauana kwa sababu ya hasira, ni hasira gani hiyo inayokufanya usiogope kutoa roho ya mwenzako,” alihoji.

Alisema timu itakayoundwa itapewa jukumu la kufanya usuluhishi na kupata maridhiano (reconciliation) kijiji kwa kijiji huku ikipeleka ujumbe wa amani.

“Tunataka kutumia Kiteto kama mradi wa majaribio (pilot project) kwenye suala la kutafuta amani kwenye maeneo kama haya,” alisema Waziri Mkuu.

Alisema wilaya ya Kiteto inaingiliana na mikoa mitano ambayo ni Tanga (Kilindi), Morogoro (Gairo); Dodoma (Kongwa) Manyara (Simanjiro) na Arusha (Monduli) hali ambayo inachangia kuwepo na muingilianio mkubwa wa kijamii.

Waziri Mkuu alitaja hatua nyingine zitakazochukuliwa na Serikali kuwa ni kupima ardhi inayogombewa yenye ukubwa wa hekta 133,000 na kuigawa kwa wafugaji ili wafuge kwa mtindo wa ranchi na inayobakia igawiwe kwa wakulima.

Kikao cha kutatua mgogoro kiteto viongozi warushiana maneno.
Wakati huo huo Serikali ya mkoa wa Manyara imeanza hatua nyingine za kutafuta utatuzi wa mgogoro wa ardhi kati ya wakulima na wafugaji unaojirudia mara kwa mara kwa kuwakutanisha viongozi wa mila kutoka jamii za kifugaji wakulima viongozi wa dini na wanasiasa kikao ambacho kimeshuhudia malumbano makali kutoka kwa baadhi ya viongozi huku wengine wakituhumiwa kuhusika katika kuchochea mgogoro huo.

Katika kikao hicho kilichoongozwa na mkuu wa mkoa wa Manyara Eraston Mbwilo kilianza kwa kutoa nafasi kwa wazee kutoka katika jamii hizo mbili ambapo kwa upande wa wakulima walitoa malalamiko ya kutoridhishwa na hatua za utatuzi zinavyo endelea na viongozi wa kifugaji wakikana kuhusika na uchochezi na kuitaka serikali ishirikiane nao kumaliza tatizo hilo.

Mbunge wa kiteto Benedict Ole Nangoro amesema wao kama viongozi wana wajibu wa kumaliza mgogoro ndani ya kiteto lakini serikali inapaswa kuongea na viongozi waliyo nje ya wilaya ambao wanahusika katika mgogoro huku mwenyekiti wa halmashauri ya kiteto Mahinge Lemalali akiomba serikali iwakutanishe na viongozi wa wilaya za jirani waongee kwakuwa malumbano kati yao yanachangia mgogoro huo